Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Gazeti la Haaretz la Israel linaripoti kuwa raia hao wa Kizayuni wamemiminika katika barabara mbalimbali za Tel-Aviv na kutangaza upinzani wao dhidi ya mpango huo wa Benjamin Netanyahu.
Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za kuulaani mpango huo na kueleza kwamba, hatua hiyo itaibua vitendo vya utumiaji mabavu na kuzidi kuvuruga amani na usalama.
Kadhalika waandamananaji hao wamelitaka baraza la mawaziri la Israel kuachana na mpango huo wa kutaka kuzipora na kuzikalia kwa mabavu ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamekubaliana kwamba, kuanzia tarehe Mosi ya mwezi ujao wa Julai watayaunganisha maeneo ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Suala hilo limepingwa vikali na jamii ya kimataifa.
Hivi karibuni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ililitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Haki za Binadamu na Mahakama za kimataifa kuchukua hatua za haraka za kusitisha utekezaji wa mpango huo wa kutwaa ardhi zaidi za Palestina huko katika Ukingo wa Magharibi.
Aidha Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan ameutahadharisha utawala wa Israel kuwa utaraji mapigano makubwa iwapo utasonga mbele na mpango wake wa kuteka zaidi ardhi za Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
342/